15th January 2015
Katika vurugu hizo, polisi wealiwatia mbaroni wanafunzi 86 wanaosoma programu maalum ya Stashahada ya Ualimu kwa tuhuma za kuhamasisha uvunjifu wa amani na kufanya maandamano.
Wanafunzi hao ni wa programu maalumu katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknohama iliyoanza mwaka jana. Wanafunzi hao waligoma kuingia madarasani jana na kufanya maandamano ya amani kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwasilisha madai yao.
Wakati wakiandamana kwa kupitia njia za pembezoni kuelekea kwa Waziri Mkuu katika eneo la Makulu, polisi walifika ghafla Jeshi la polisi liliwatawanya kwa mabomu ya machozi na hivyo kushindwa kufika katika ofisi hiyo. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, David Misime, wanafunzi hao walifanya maandamano hayo majira ya saa 11:30 alfajiri jana.
Alisema wanafunzi hao walikuwa na malengo ya kuelekea katika ofisi mbalimbali za viongozi wa serikali zilizopo mjini Dodoma. Alisema chanzo cha wanafunzi kugoma ni kutokana na maamuzi waliyokubaliana katika kikao chao walichofanya cha tarehe juzi wakidai kuongezewa posho ya chakula na kwamba hata kiasi ambacho wanapewa wamechelewa kupewa.
“Hata hivyo uongozi wa chuo uliwaeleza kuwa wenye mamlaka ya kuzungumzia suala la kuongezewa posho ni Bodi ya Mikopo na siyo chuo, hivyo walitakiwa kufuata taratibu za kuwasilisha madai yao pia walielezwa kuwa hundi kwa ajili ya fedha za posho zao zimeshasainiwa na kuwasilishwa benki ili waweze kuanza kupewa posho zao,” alisema Misime.
Alisema hata hivyo, wanafunzi hao hawakuridhika na usiku wakaanza kuhamasishana kufanya maandamano, jambo ambalo ni kosa. Alisema ushahidi wa awali wa meseji, vipeperushi na vikao visivyo halali mahakamani kwa kosa la Kufanya maandamano yasiyo na kibali.
“Endapo wataendelea kufanya hivyo, wasije wakalilaumu Jeshi la Polisi kwani hatua zitachukuliwa bila kujali wao ni wanafunzi wa vyuo vikuu kulingana na sheria inavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,” alisema Misime.
Wakizungumza jana na NIPASHE kwa nyakati tofauti, wanafunzi hao walidai sababu zilizowafanya kugoma na kuandamana ni hali ngumu ya maisha chuoni hapo kutokana na uongozi wa chuo kutowalipa fedha zao za malazi, chakula, vitabu na viandikwa ambazo walitakiwa kupatiwa Januari 6, mwaka huu.
“Tumeamua kugoma na kuandamana kwa lengo la kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu kupeleka malalamiko yetu, kama Serikali ilikuwa haijajipanga kwa ajili ya kutusomesha ni bora waturuhusu turudi kwanza nyumbani kuliko kuendelea kuteseka na njaa hapa chuoni,” alisema mmoja wa wanafunzi ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Wakifanunua madai yao walisema kwa mujibu wa barua zao za kuitwa kujiunga na Udom, waliambiwa kuwa Serikali itagharamimia gharama zote ikiwa ni pamoja na ada, chakula, malazi, vitabu na viandikwa.
Hata hivyo, walisema walikuwa wanayapeleka madai yao Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuchelewesha malipo yao, kukatwa malipo bila kupewa risiti, kupewa ufafanuzi juu ya tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano kuwa watapatiwa mkopo asilimia 100 kwa kozi hiyo maalum.
Walisema kutokana na tamko hilo, kila mwanafunzi anapaswa kulipwa Sh. 10,000 kwa siku. Walitaja madai mengine kuwa ni malipo wanayosainishwa na chuo ya Sh. 6,000 kwa siku nayo kuendelea kukatwa badala ya kulipwa Sh. 367,500 kwa miezi miwili, lakini wanalipwa Sh. 226,500.
“Kutokana na barua hizi tulijua Serikali itatusaidia kutupatia elimu bila matatizo, hivyo tulifika chuoni hapo tukiwa na akiba kidogo tulizopewa kutoka kwa wazazi wetu, lakini kwa sasa tumeishiwa kabisa,” alieleza mwanafunzi mwingine bila kutaka jina lake kutajwa.
Walibainisha kuwa walishapeleka malalamiko yao kwa uongozi wa chuo, lakini wameshindwa kuwasaidia na kadri siku zinavyozidi wanakumbana na hali ngumu ya maisha.
Walisema uongozi wa chuo baada ya kusikia kuwa jana watagoma na kufanya maandamano, waliingiza malipo kwa wanafunzi 392 kati ya 2,000.
NIPASHE ilimtafuta Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula, ili kuzungumzia madai hao, lakini simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alijibu kuwa alikuwa katika kikao, hivyo atafutwe baadaye. Hadi tunakwenda mitamboni, Prof. Kikula hakupatikana kutoa ufafanuzi huo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment